KWAKO,
Emmanuel Mgaya ‘Masanja’. Naamini u mzima na unaendelea vyema na
majukumu yako ya kila siku. Kwa upande wangu nipo sawa, nakimbizana na
maisha.
Nina machache ya kukushauri kuhusiana na maisha yako kama staa ambaye
kwa sasa umetangaza kuokoka. Kwa maneno mengine ni kwamba, umeondoka
kwenye utaifa, upo mikononi mwa Muumba wako.Nimekufahamu kwa kitambo
kidogo. Kwangu mimi, wewe ni mmoja wa mastaa wa ukweli katika
uchekeshaji Bongo. Mwenye kipaji cha hali ya juu na unayejua
unachokifanya.
Tatizo ni kwamba, nashangazwa na aina ya maisha yako baada ya
kutangaza kuokoka. Ninavyojua mimi, kuokoka ni kuachana na maisha ya
awali ambayo (pengine) yalikuwa hayampendezi Mola na kugeukia katika
maisha safi.Niliposikia umeokoka nilifurahi kuona kuwa umeelekea sehemu
sahihi zaidi kiimani. Lakini moyoni nilikuwa na shaka kidogo maana wapo
wasanii wengi kwenye uigizaji ambao walitangaza kuokoka lakini baadaye
wakaonekana kwenye njia zao za awali.
Ukiachana na waigizaji, pia kuna wasanii wa Bongo Fleva ambao nao
waliingia kwenye ulokole na mara wakaamua kurudia maisha yao ya
awali.Baadaye nikasikia kuwa unasomea Uchungaji (ingawa inaelezwa kuwa
ni Uinjilisti), hapo sikuwa na shaka tena na wokovu wako. Niliamini kwa
mtu ambaye ameamua kuingia kwenye kufundisha wengine njia iliyo sahihi
hawezi kudanganya kuwa ameokoka.
Siyo kama naingilia maisha yako au nakukosoa kwenye suala la imani
yako. Uzuri ni kwamba, nami ninaamini katika imani yako, hivyo sioni
tatizo kukushauri.Tatizo lipo kwenye staili yako ya maisha. Ni kweli
kwamba umeokoka, lakini itawezekana vipi usuke mabutu kichwani? Maandiko
yanaeleza wazi kuwa, wanaoamini ni barua inayosomeka kwa watu wote.
Je, watu watasoma nini kupitia mabutu? Unaweza kusema kuwa, imani ya
mtu iko moyoni, hapo sitakubaliana na wewe, maana kinachoonekana nje,
kinawakilisha kilichomo ndani.Vipi kama kanisa zima, wanaume wataingia
wamesuka? Nafikiri si jambo sahihi. Watu watapata shaka na wokovu wako,
tena mchunga kondoo. Wengine wanaweza kuona wokovu si jambo ‘serious’.
Kwamba mtu anaweza kuingia na akaendelea na mambo yake yaleyale, jambo
ambalo si la kweli.
Wokovu ni pamoja na mwonekano wa nje. Mavazi, mitindo ya nywele
n.k.Jambo jingine ambalo limenishangaza ni namna unavyoingiza komedi
kwenye mambo yanayohusu dini.Usahihi wa kufanya utani kwenye vichekesho
huku ukitaja jina la Mungu unatokea wapi? Masanja tumezuiwa kufanya
mzaha au kulitaja bure Jina la Mungu wetu.
Nakushauri kama ni kweli umeamua kuokoka, badilika lakini kama
unahisi bado unatamani maisha ya kawaida na kujichanganya, chagua moja
ili jamii isikutafsiri tofauti.Ni uamuzi wako kufuata au kuacha
hapahapa, lakini la muhimu ni kwamba, nitakuwa nimeshakushauri.
Ubarikiwe sana mpendwa!
Yuleyule,
Mkweli daima,
.........................
Joseph Shaluwa.
BARUA NZITO KWA MSANII WA ORIJINO KOMEDI BONYEZA HAPA USOME

No comments: