Baada ya kuwa katika mapenzi na mwanaume huyo kwa zaidi ya miaka 17,
wakipendana na kuitana majina yote mazuri unayoyajua yakiwamo kuambiwa
‘mpenzi wangu nakupenda, nikinywa maji nakuona kwenye glasi’…leo mapenzi
yamegeuka shubiri.
Kuna mikasa mbalimbali huwatokea watu katika suala zima la mapenzi,
kiasi cha kusababisha baadhi yao kutopenda tena kuingia kwenye jambo
hilo wakiliona kama ni kitu kisichofaa, ingawa ukweli unaweza kuwa sio
huo.
“Sitaki tena wanaume, ni watu wabaya, wameniumiza moyo wangu mno,”
anasema Hawa Francis, mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam. Sababu kubwa ni
kero ambazo amewahi kuzipata katika suala zima la uhusiano. Vivyo hivyo
wapo wanaume hawataki kuoa, kwa maelezo kuwa kuna wanawake wamewahi
kuwatesa.
Kama wewe ni kati ya watu ambao umekata tamaa na suala la uhusiano,
fahamu kuwa si wewe pekee.Kuna kundi kubwa la watu wameshatendewa kiasi
cha kufanya wasiwe na raha tena.
Mkasa wa mwanamke kukatwa mkono
Ilikuwa Agosti 7, mwaka huu, saa mbili usiku. Ilikuwa ni siku
iliyobadili historia ya maisha yake. Baada ya kuwa katika mapenzi na
mwanaume huyo kwa zaidi ya miaka 17, wakipendana na kuitana majina yote
mazuri unayoyajua yakiwamo kuambiwa ‘mpenzi wangu nakupenda, nikinywa
maji nakuona kwenye glasi’…leo mapenzi yamegeuka shubiri.
Mwanamke huyo, Mchali Kihiyo (35), mama wa watoto sita, aliyepoteza
viungo vyake kutokana na ukatili wa kijinsia uliofanywa na mwanaume
ambaye wamekuwa na uhusiano nae (jina limehifadhiwa).
“Uhusiano wetu ulikuwa mzuri, hata hivyo kwa sasa naona mambo yamekuwa
magumu kwangu, leo hii mimi sina mkono wa kushoto na nimeondolewa sehemu
ya viungo vyangu vya upande mmoja,”anasema Mchali,akibubujikwa machozi
kutokana na ulemavu alioupata.
Chanzo cha ulemavu
Anasema maisha yao ya uhusiano yalikuwa ya furaha kwa kipindi chote
lakini yamegeuka shubiri baada ya mwanamume wake huyo kuonyesha dalili
ya kutompenda kama awali, hali ambayo anaitafsiri kama labda alikuwa na
mwanamke mwingine.
Mchali, anasema mikasa na mateso ilianza miaka mitatu iliyopita baada ya
kuhisi kwamba mwanamume wake huyo amezaa na mwanamke mwingine. Ubaya
zaidi ulimtokea baada ya mtoto wa huyo mwanamke mwingine, kutumbukia
kwenye kisima cha maji na kisha kupoteza maisha.
“Kifo cha mtoto huyo, ndicho kilichozaa tatizo hili la ukatili dhidi
yangu na kunisababishia ulemavu, kwa kuwa huyo mwanaume wangu na huyo
mwanamke aliyezaa nae, walidai kwamba mimi ndiyo nilimtupia majini
marehemu mtoto wao ili afe,”anasema mama huyo.
Vitisho kabla ya ulemavu
Mchali, anasema mara baada ya msiba wa mtoto kumalizika, mwanamume wake
huyo alihamia kwa mke mdogo lakini akawa anarejea nyumbani na kumtukana
huku akitishia kufanya lolote analofikiri linafaa.
Anasema baada ya mateso na vitisho kuzidi aliamua kuondoka kwa mumewe
huyo toka mwezi Aprili mwaka huu na kuamua kurudi kwa wazazi wake huku
akiwaacha watoto wake kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi.
Anasema alilazimika kuwaacha watoto kutokana na agizo la mumewe,
aliyekataa asiwachukue, hivyo akaanza maisha mengine ya upweke bila
watoto huku akiendesha maisha yake kwa biashara ya kuuza samaki.
Anasema mwanzoni mwa mwezi huu, aliugua malaria na kukaa nyumbani bila
kwenda kwenye biashara zake. Agosti saba mwaka huu, alipata nafuu na
kuamua kwenda kumsalimia kaka yake, anayeishi mbali kidogo na nyumbani
kwao na ndipo yakamkuta yaliyomkuta.
Anaeleza kuwa alikaa kwa kaka yake hadi muda wa futari wakafuturu na
kushangaa simu yake ikiita, kuangalia ni namba ya mpenzi wake huyo.
Alipoipokea, aliulizwa aliko, yeye alimweleza yuko kwa kaka yake na
kumtaka amfuate mnadani akale nyama kitendo ambacho anasema alipingana
nacho.
Anasema baadaye aliamua kurudi nyumbani na kusindikizwa na wifi yake
hadi karibu na nyumba yao ikiwa ni saa mbili usiku.Walipoagana, ghafla
akashangaa kusikia sauti ya mumewe ikimuita, alipogeuka alimwona, kisha
akamuuliza alikotoka na kumwambia alikuwa kwa kaka yake.
Kipigo na ulemavu
Anasema mara baada ya kumjibu mwanamume huyo alianza kumpiga na hatimaye
alianguka chini na mumewe akatoa panga na kuanza kumkatakata sehemu
mbalimbali za mwili wake.
Hakika hujafa hujaumbika. Mchali amecharangwa kwa mapanga kuanzia chini
ya goti mguu wa kushoto hadi kwenye makalio, amekatwa sehemu zaidi ya
saba mwilini.
Ni kama alitaka kumkata shingo
Anasema kwa namna anavyoona ni kama alidhamiria kumuua akisema kuwa mara
nyingi akiwa na huo upanga alikuwa analenga kumtenganisha shingo.
Alichofanya mama huyo ni kuweka mikono shingoni kuzuia panga, kitendo
kilichosababisha mkono wake wa kushoto kukatwa kabisa.
Hawezi kukaa
Mwandishi wa makala haya baadaye alimwomba mwanamke huyo angalau akae
chini, kwani muda mwingi wa mahojiano alikuwa amelala, ndipo alipojibiwa
kwamba hawezi kukaa kwa vile kuna nyama kubwa kwenye makalio ambayo
imeshindikana kushonwa.
Mama huyo anasema wakati mumewe akimcharanga mapanga, mama yake mzazi
aliendelea kupiga ngolo (yowe) kuomba msaada, kaka yake alikwenda lakini
akashindwa kutoa msaada kwa kuwa shemeji yake huyo alikuwa akimkimbiza
na panga.
Anasema kelele za mama yake zilisaidia kuokoa maisha yake, kwa kuwa
majirani walijitokeza, hivyo mwanamume huyo akaanza kuwakimbiza akitaka
kuwadhuru kitendo ambacho mama huyo aliona ndiyo nafasi pekee kukimbilia
ndani.
Matibabu
Mchali, anasema baadaye ndugu zake, walitafuta usafiri na kufanikiwa
kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako alilazwa kwa
siku nne na kurejea nyumbani kutokana na ushauri wa daktari
anayemhudumia.
Kwa mujibu wa mama huyo, daktari anayemtibu alimtaka Mchali akubali
kutibiwa majeraha akiwa nyumbani ili kuepuka maambukizi ya magonjwa
nyemelezi pamoja na kuepuka gharama za matibabu.
“Sina uwezo wa kukabiliana na gharama za matibabu kwa kuwa siwezi
kutembea, nalazimika kukodi gari na kwa wiki naoshwa mara tatu.
Nisaidieni ndugu zangu, ndoa yangu imenifikisha hapa,” anasema.
Mchali na hali ya ukatili mkoani Manyara
Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa anasema mtuhumiwa bado
hajakamatwa kwa vile hajulikani aliko, huku akiahidi kuendelea
kulifanyia kazi suala hilo.
Akielezea zaidi ukatili mkoani Manyara, anasema upo, japo ni mdogo
ikilinganishwa na mikoa mingine. Anaamini kuwa bado changamoto ni kubwa
kwa wanawake ambao wengi wao wamekuwa wakinyanyasika.
Sababu kubwa za kunyanyasika kwa wanawake ni mfumodume. Akasisitiza kuwa
Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kuelimisha jamii madhara ya
ukatili na kusema jitihada hizo zinapaswa kuigwa na wananchi na asasi
nyingine kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatokomezwa.
Soma zaidi: http://mwanahabariuswazi.blogspot.com/2013/09/ukatili-wa-kutishamke-akatwa-mkono-na.html#ixzz2eUUOMgzz
No comments: