RAIS Jakaya Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwafikisha
mbele ya vyombo vya haki watu wote waliohusika katika ulipuaji bomu
lililosababisha kifo na kujeruhi watu saba mjini Unguja, Zanzibar.
Kikwete ambaye amesema kitendo hicho ni cha kulaaniwa kwa nguvu zote na
watu wote wapenda amani Bara na Visiwani, amekitaja kuwa ni cha woga
kisicho na ustaarabu, kisichokubalika katika dunia ya sasa.
Alisema hayo katika salamu za rambirambi alizotuma jana kwa Rais Ali Mohamed Shein wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Bomu hilo lilirushwa katika shughuli ya kidini iliyokuwa ikifanyika
katika eneo la Darajani , mjini Unguja. Miongoni mwa majeruhi, yumo
mhubiri wa amani ajulikanaye kama Sheikh Ahmed Haidari Jabir wa
Zanzibar.
“Hicho ni kitendo cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu wote wapenda
amani Bara na Visiwani, ni kitendo cha woga na kisicho na ustaarabu na
wala hakikubaliki katika dunia ya sasa,” alisema. Rais Kikwete
aliongeza,
“Hiki ni kitendo kilichofanywa na watu waoga, wasio na ustaarabu wa aina yeyote ile.”
Alikemea wanaofanya vitendo hivyo na akahimiza watu kuwa wastaarabu,
wavumilivu na kuheshimu imani na mitizamo ya watu wengine hata kama
hawakubaliani nao.
Akiendelea kulaani, alisema amesikitishwa zaidi na watu hao wasio na
ustaarabu ambao wamefanya kitendo hicho cha kihalifu kwenye shughuli ya
kidini ambapo ndipo mahali panapostahili amani, uvumilivu na unyenyekevu
zaidi kwa kuwa ni wakati ambapo binadamu anapofanya mawasiliano na
muumba wake.
Alihimiza polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki
wahusika wa tukio hilo. Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na
Makosa ya Jinai wa Zanzibar, Yussfu Ilembo, aliyekufa papo hapo ni
Muhammad Mkombalaguha (26), mkazi wa Tanga.
Kutokana na tukio hilo, polisi visiwani humo ilitangazia hali ya hatari
watu waliohusika na shambulio hilo. Ilielezwa kwamba uchunguzi umeanzia
kwenye mabaki ya vitu vilivyokutwa katika eneo la tukio.
Miongoni mwa vielelezo vilivyokusanywa ni pamoja na vipande vya mabaki
ya gundi ya karatasi na vitu vingine ambavyo vinasadikikwa vimetumika
kutengeneza bomu hilo.
Mtu aliyekufa pamoja na majeruhi, walikutwa na mkasa huo wakati wakitoa
Msikiti wa Darajani baada ya Ibada ya Swala ya Isha inayoswaliwa kuanzia
saa 1:45 usiku na kuendelea.
Baada ya kumalizika ibada hiyo, walitoka msikitini na kufika eneo la
Darajani wakisubiri gari na ndipo mlipuko mkubwa uliposikika ambao
unasadikiwa kuwa ni bomu.
Amani, uzalendo Katika hatua nyingine, akiwa mkoani Dodoma juzi, Rais
Kikwete aliwataka Watanzania kuendelea kulinda na kupigania amani
iliyopo kwa ustawi na usalama wa nchi .
Rais Kikwete alisema hayo juzi kwenye uzinduzi wa tamasha la uzalendo
lililoasisiwa na wasanii wa muziki na filamu nchini ikiwa ni pamoja na
uzinduzi wa video ya wimbo maalumu wa Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
Alisema uzalendo kwa Watanzania ndiyo njia pekee ya kufanya taifa liendelee kutunukiwa hadhi ya kisiwa cha amani duniani.
Katika tamasha hilo lililofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Rais
Kikwete alisema ili kuwaenzi waasisi wa taifa, ni lazima kudumisha
misingi ya amani na kujitolea kizalendo kulilinda na kulitetea taifa
kama walivyofanya waasisi Mwalimu Julius Nyerere na Shehe Abeid Amani
Karume.
Pia aliwataka wasanii kutumia vizuri talanta walizojaliwa kufikisha ujumbe wenye uzalendo kwa Tanzania.
No comments: