Wanajeshi
wa Brigedi Maalum wakiwa katika mazoezi makali yaliyofanyika hivi
karibuni huko Goma Mashariki ya Demokrasia ya Kongo..
Mmoja
wa walinda amani kupitia Brigedi Maalum inayoundwa na wanajeshi kutoka
Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi akiwa katika moja ya mazoezi
yaliyofanyika hivi karibu huko Goma.
Kamanda Mkuu wa Misheni ya Kulinda
Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ( MONUSCO ) Luteni
Jenerali Carlos Albeto dos Santos Cruz ametakanza jana jumanne akiwa
Goma kwamba MONUSCO itaanza rasmi kuitumia Brigedi Maalum na ametoa saa
48 kuanzia saa kumi jioni kwa saa za Goma jana siku ya Jumanne waasi
wote kusalimisha silaha zao, na kwamba ifikapo saa kumi jioni kwa saa za
Goma siku ya Alhamisi Agosti Mosi wale wote ambao watakuwa
hawajasalimisha silaha zao watachukuliwa kama tishio la usalama kwa
wananchi na MONUSCO italazimika kuwapokonya ikiwa ni pamoja na kutumia
nguvu kwa mujibu wa Mamlaka iliyopewa na Sheria zinazowaruhusu kufanya
hivyo.
------------------------------
Misheni
ya Kutuliza Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (
MONUSCO) imetangaza kwamba kwa mara ya kwanza itaanza kuitumia Brigedi
Maalum ( Force Intervention Brigade) katika kudhibiti eneo maalum
la usalama ( security zone ) kuzunguka mji wa Goma ulioko Mashariki
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na imewapa saa 48 waasi
kusalimisha silaha zao.
Taarifa
iliyotolewa na MONUSCO na kusambazwa na Idara ya Mawasiliano ya Umoja
wa Mataifa jana jumanne, inaeleza kwamba watu binafsi katika eneo la
Kivu ya Magharibi ambalo linajumisha Goma na Sake na ambao
hawahusiki na vyombo vya usalama watapewa saa 48 kuanzia saa kumi jana
kwa saa za Goma ( Jumanne ) kuzisalimisha silaha zao katika Misheni
hiyo na kujiunga na mchakato wa DDR/RR unaoratibu upokonyaji,
usambaratishaji, urejeshwaji makwao, kuwaunganisha na jamii na
kuwapatia makazi.
Baada ya saa kumi
jioni ya Alhamisi, Agosti Mosi. Taarifa hiyo inasema. Wale wote ambao
watakuwa hawajasalimisha silaha zao watachukuliwa kama tishio kwa
usalama wa wananchi na MONUSCO itachukua hatua zote muhimu kuwapokonya
silaha hizo ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu kama ilivyoainishwa katika
Mamlaka na sheria za ushiriki za MONOSCO.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo zaidi ya wananchi milioni moja wanaishi katika
eneo dogo la Goma na Sake na kando kando ya barabara ambayo
inawaunganisha na kambi ya wakimbizi ya Mugungu ambayo ni makazi ya
muda ya watu karibu 70, 000 ambao wameyakimbia makazi yao kutokana na
mapigano.
Kwa mujibu wa MONUSCO,
tangu kati kati ya mwezi Mei eneo hilo limeshuhudia mapigano ya mara kwa
mara kutoka kwa kundi la M23 dhidi ya majeshi ya Serikali ya FARDC
ikiwa ni jaribio la wazi la kutaka kusonga mbele kuelekea Goma na
Sake.
“
Katika mashambulizi hayo, likiwamo la hivi karibuni la Julai 14, M23
walitumia kiholela silaha zao za moto zikiwamo silaha nzito ambazo
zimesababisha wananchi kujeruhiwa” .
Taarifa hiyo imeongeza kwamba kundi hilo la M23 katika mashambulizi hayo limelenga pia Vituo vya Umoja wa Mataifa.
Aidha
taarifa hiyo inabainisha kwamba eneo hilo maalum la usalama ( security
zone) litasaidia kudhibiti tishio la moja kwa moja mbali na eneo la
nje ya Goma na pengine eneo hilo linaweza kupanuliwa na kurudiwa
sehemu nyingine kutakako hitajika.
Tamko
hilo la kutoa saa 48 kwa waasi kusalimisha silaha zao linafuatia
kuwasili katika eneo la Goma kwa Kamanda Mkuu wa MONUSCO, Luteni
Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz, ambaye alitangaza kwamba
Misheni ya MONUSCO itaunga mkono jeshi la Serikali ( FARDC) katika
kuanzisha eneo la usalama kuzunguma eneo la Goma na vitongoji vyake.
Taarifa
hiyo inamkariri Kamanda Mkuu wa MONUSCO akiyapongeza majeshi ya
serikali kwa kazi nzuri iliyofanya wiki iliyopita ya kuwadhibiti M23.
Ingawa anasema eneo la Goma na Sake bado limo katika mazingira
magumu sana na kwamba ni wajibu wa wahusika wote kuhakikisha wahalifu
wote hawaendelei kuhatarisha raia wa eneo hilo.
Kwa
mwaka uliopitia , kundi la M23 pamoja na makundi mengine yenye silaha
yamekuwa yakipambana mara kwa mara na majeshi ya serikali katika
Mashariki ya Kongo, huku makundi hayo yenye silaha mwezi Novemba mwaka
jana yakiikalia Goma kwa muda.
Aidha
mapingano ya hivi karibuni ambayo safari hii yalihusisha pia kundi
jingine la wanagambo wenye silaha lenye asili yake nchini Uganda,
yamesababisha zaidi ya wananchi 100,000 kuyakimbia makazi yao na hivyo
kuongeza mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo linalohusisha watu
wengine 2.6 milioni ambao wameyakimbia makazi yao huku wengine 6.4
milioni wakihitaji chakula na huduma za dharura.
Wakati
huo huo, Kaimu Mkuu wa MONUSCO Bw. Moustapha Soumare katika
taarifa yake ametoa wito kwa pande zote kutafuta suluhu ya kisiasa
kwa matatizo ya DRC kupitia Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa
Mataifa kuhusu amani, usalama na ushirikiano wa maendeleo katika DRC
na eneo la Maziwa Makuu uliopitisha mwezi wa Februari na viongozi 11
wa Afrika na Taasisi nne za Kikanda na Kimataifa.
Aidha akasema katika kipindi hiki ambacho suluhu la kisiasa linatafutwa MONUSCO itatumia nguvu iliyonayo kuwalinda wananchi dhidi ya hatari zitokanazo na makundi ya waasi.
No comments: