Ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere*Matajiri wauteka, waharibu mfumo wa ukaguziMFUMO wa ukaguzi wa wasafiri na mizigo
yao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
umetekwa na sasa uko mikononi mwa matajiri na wanasiasa wanaofanya
biashara ya dawa za kulevya hapa nchini, MTANZANIA Jumapili linaandika
kwa uhakika.
Vyanzo vya habari vya kuaminika vilivyo
ndani ya serikali vinavyofanya kazi bega kwa bega na dawati la habari za
siasa na uchunguzi la MTANZANIA Jumapili vimedokeza kuwa, baadhi ya
watoto wa viongozi wakuu wa nchi, wafanyabiashara wenye ukwasi wa
kutisha na wanasiasa wenye utajiri ambao umekuwa ukitiliwa shaka kwa
muda mrefu, wamebainika kuingilia mfumo wa kiitelejensia wa JNIA kwa
kuupandikizia watu ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa maelekezo yao.Ripoti ya uchunguzi wa kikachero iliyo mikononi mwa maofisa wa juu serikalini na ambayo waliinukuu katika mazunguzo yao na gazeti hili, inaeleza kuwa mtandao wa matajiri wauza dawa za kulevya umewaondoa wafanyakazi kadhaa watiifu waliokuwa katika kitengo cha ukaguzi wa abiria na mizigo cha JNIA na kupachika watu wao walio kwenye mfumo wa malipo wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Sambamba na hilo, walieleza kuwa kitengo cha kupambana na biashara ya dawa za kulevya nchini kimedhoofishwa na hata mbwa wa polisi waliokuwa wakitumika kukagua mizigo ya wasafiri wanaotumia uwanja wa JNIA wameondolewa katika mfumo wa ukaguzi na sasa watumika kwa nadra, hasa zinapovujishwa taarifa za usafirishaji wa dawa za kulevya ambazo hutolewa aghalabu wafanyabiashara hao wanapohitilafiana kibiashara na kuamua kuumbuana.
Taarifa hizi zimethibitishwa na kauli ya Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP) Godfrey Nzowa, ambaye katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumapili, alieleza kuwa mtandao wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya hapa nchini una pesa nyingi zinazouwezesha kufanya jambo lolote ili kufanikisha biashara hiyo.
Kamishina Nzowa, ambaye alitakiwa na gazeti hili kutoa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na matukio hayo ya dawa za kulevya, likiwemo lile la Watanzania wawili waliokamatwa nchini Afrika Kusini wakiwa na kiasi kikubwa cha dawa za kulevya pamoja na uwezo wa kitengo chake wa kupambana na wauza dawa za kulevya, alisema kazi hiyo ina changamoto kubwa katika kufanikiwa kwake, kwa sababu inawahusisha watu wenye fedha nyingi hapa nchini.
Alisema, Watanzania wawili, Agnes Gerald (25) na Melisa Edward (24), waliokamatwa na kilo 150 za dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo nchini Afrika Kusini, Julai 5, mwaka huu, walifanikiwa kupita JNIA bila kugundulika kutokana na watu waliokuwa kwenye mashine za ukaguzi wa abiria na mizigo.
“Hawa Watanzania waliopita kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere na kukamatwa Afrika Kusini, waliweza kupita kwa sababu inategemea na watu waliokuwepo kwenye mashine za ukaguzi siku hiyo. Unajua hakuna ushirikiano wa karibu baina ya watendaji wanaohusika na udhibiti wa dawa za kulevya. Hilo ni tatizo kubwa linalosababisha vikwazo katika kupambana na mtandao wa dawa hizo.
“Sisi tunategemea kupata taarifa za wauza dawa za kulevya kutoka kwa watu, wakiwemo wakaguzi wa mizigo na abiria, hapo ndipo tunakwenda kumpekua mtu anayeshukiwa kubeba dawa hizo. Tunapopewa taarifa tunafanya ukaguzi, mbwa tunawanusisha, lakini mara chache kwa sababu wakati mwingine wanashindwa kugundua mizigo yenye dawa hizo iliyopuliziwa manukato au kunyunyiziwa kahawa,” alisema Nzowa.
Kamishina Nzowa pia alilalamika kukithiri kwa rushwa kwa watendaji ndani ya kikosi cha kupambana na dawa za kulevya pamoja na jamii kuwa ni jambo ambalo linasababisha kushamiri kwa biashara hiyo.
Mbinu mpya za kusifirisha dawa za kulevya
Duru za uchunguzi za MTANZANIA Jumapili,
zimebaini kuwepo kwa mbinu mpya inayotumiwa na wafanyabiashara wa dawa
za kulevya kusafirisha mizigo yao tofauti na ile iliyozoeleka.
Wafanyabiashara, wanasiasa na watoto wa
viongozi wa serikali wanaojihusisha na biashara hiyo sasa wameligeukia
kundi la wasanii wa filamu na wanamuziki wa kizazi kipya wanaotajwa kuwa
na tamaa ya utajiri wa haraka haraka na kulifanya wasafirishaji wakuu
wa dawa hizo.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, wasanii
hususan vijana, ndio wanaotumiwa zaidi kubeba dawa za kulevya huku
wakihakikishiwa usalama wao na matajiri na wanasiasa wanaotajwa kuwa
karibu na baadhi ya viongozi wa serikali wanaowatumia kama kinga yao,
kwa makubaliano ya kugawana kipato kinachotokana na biashara hiyo au
kuwa katika orodha ya malipo maalumu.
Mbinu zinazotajwa kutumika kusafirisha
dawa za kulevya ni pamoja na mzigo baada ya kufungwa hunyunyiziwa
pilipili, manukato au kahawa ambazo huondoa uwezo wa mbwa wenye mafunzo
maalumu ya kutambua dawa za kulevya kubaini.
Imebainika kuwa dawa za kulevya
zilizofungwa vizuri na kunyunyiziwa unga wa pilipili au kahawa juu yake
huondoa uwezo wa mbwa kunusa harufu kwa usahihi na badala yake humfanya
apige chafya.
Njia nyingine inayotajwa ni kufunga dawa
za kulevya ndani ya karatasi ya kaboni ambayo mashine za ukaguzi zilizo
katika uwanja wa ndege hazina uwezo wa kubaini kilichofungwa ndani
pamoja na uvaaji wa nguo maalumu za ndani za wanawake zinazofahamika
zaidi kwa jina la ‘tight’ zilizoshonewa dawa za kulevya ndani ambazo
hazitambuliwi kirahisi na maofisa wa ukaguzi, bali humuonyesha mwanamke
akiwa amejazi
TAA wagwaya
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege (TAA), Mhandisi Suleiman S. Suleiman, alipoulizwa na MTANZANIA
Jumapili namna mamlaka yake inavyokabiliana na tishio la ongezeko la
upitishaji dawa za kulevya JNIA, alikataa kuzungumza lolote kwa kile
alichoeleza kuwa kufanya hivyo ni kuathiri mwenendo wa uchunguzi
unaoendelea.
Source:Mtanzania
Source:Mtanzania
No comments: