MBUNGE
wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, amesema yupo tayari kujiuzulu ubunge,
ikiwa itabainika anajihusisha biashara ya dawa za kulevya. Kauli hiyo
imekuja siku chache baada ya kutajwa katika moja ya barua iliyosambazwa
katika mitandao ya kijamii, baada ya mtu anayedaiwa kukamatwa China na
kuwatuhumu watu kadhaa akiwamo Idd Azzan. Akizungumza
na MTANZANIA jana kuhusu sakata hilo, alisema hatua ya kuhusishwa na
biashara haramu ya dawa za kulevya, ni kutotenda haki mbele ya jamii
hasa wapiga kura wake na Taifa kwa ujumla.
Alisema mtu aliyendika barua ya tuhuma dhidi yake, ni wazi amedhamiria kumshushia heshima na huenda akawa ana jambo limejificha.
“Ni kweli nimeiona hiyo barua katika mtandao, inayodaiwa imeandikwa na
kijana ambaye amekamatwa Hong Kong nchini China. Lakini ninajiuliza kama
kweli yeye ni raia mwema, katika hili kwanini hakutaka kutaja jina lake
kwenye barua hiyo.
“Hata nilipoisoma nimebaini kuwa huyo mtu ametumika na huenda kabisa
hayupo nje ya nchi, kwani katika maelezo yake anataja jina la Balozi
Philip Marmo kuwa amemsaidia hali ya kuwa hivi karibuni Rais Kikwete
alimteua Balozi mpya Abdulrahman Shimbo na Marmo kuwa Balozi wa
Shirikisho la Ujerumani.
“Kingine naona alijaribu kuandika uongo kuweza kuaminisha jamii, kwani
hata hilo jila la balozi mwanzo limetajwa jina la Bernad na kukatwa kwa
wino. Ninapenda kulieleza Taifa kuwa naomba vyombo vya usalama vifanye
uchunguzi wa jambo hili na nikibainika ninauza dawa za kulevya nipo
tayari kujiuzulu ubunge wangu.
“Kubwa haki itendeke katika kufanya uchunguzi wa jambo hili, ila ni
lazima jamii na Watanzania kwa ujumla tusikubali kwa makusudi watu
waichafue nchi yetu kwa chuki na fitna tu,” alisema Azzan.
Alisema kutokana na hali hiyo, anashindwa kuchukua hatua yoyote ya
kufanya zaidi ya kuliandikia barua Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi
dhidi ya barua hiyo kuweza kubaini ukweli wa jambo hilo.
“Sijawahi kuuza dawa za kulevya na hata katika familia yangu hakuna mtu
anayefanya biashara hiyo haramu. Kila mmoja anajua kuwa Idd nilikuwa
Diwani wa Kata ya Magomeni, huku kazi yangu kubwa ikiwa ni biashara ya
magari na daladala ambayo ninaendelea nayo hadi sasa mbali ya ubunge
kama nilivyopewa heshima na wapiga kura wangu wa Kinondoni,” alisema
Azzan.
MTANZANIA ilipomuuliza kuwa ni hatua gani ikibainika hakuna ukweli wa
jambo hilo baada ya vyombo vya usalama kufanya uchunguzi, alisema
atakachokifanya anamuachia Mungu.
“Ni ngumu kusema hatua gani nitachukua ikibainika hakuna ukweli, lakini
nataka kusema kama yule aliyeandika barua hii angetaja jina lake ni wazi
baada ya uchunguzi ningeweza kuomba ushauri kwa mwanasheria wangu hatua
za kuchukua, lakini kwa kuwa hakutaja jina ni ngumu kuweza kuamua,”
alisema Azzan.
Kwa mujibu wa taarifa zilitolewa kupitia mitandao, ziliripoti kukamatwa
kwa Watanzania wawili nchini China wakiwa na dawa za kulevya zenye
thamani ya Dola milioni 3.34 za Marekani.
No comments: